Uongozi wa Simba SC umetoa taarifa za kuwa umepokea taarifa ya kuvunjika kwa mkataba kati ya Klabu na mchezaji wao Dejan Georgijevic.
Vilevile uongozi wa Simba SC umesema kuwa upo mbioni kumfikisha mbele ya vyombo vya sheria Mshambuliji kutoka nchini Serbia Dejan Georgijevic ‘Mzungu’, kufuatia kitendo cha kuvunja mkataba bila kufuata utaratibu.
Dejan alithibitisha kuachana na Simba SC jana Jumatano (Septemba 28) kupitia ukurasa wake wa Instagram, huku akieleza mkataba wake umevunjwa kutokana na kushindwa kutimiziwa baadhi ya makubaliano.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC Ahmed Ally, amesema Klabu hiyo itachukulia hatua stahiki Mshambuliaji huyo, ambaye jana aliamua kuondoka kambini Zanzibar, baada ya kutoa taarifa za kuvunjwa kwa mkataba wake kupitia mitandao ya kijamii.
“Tunakiri tumeziona taarifa za Dejan kuvunja mkataba, zimetusikitisha kwa sababu mchezaji kama yeye alitakiwa kufuata taratibu, kutokana na uzoefu alionao katika soka la kisasa.” “Msimamo wa Simba SC kwenye hili sisi tunakwenda kuchukua hatua stahiki kwa Mchezaji kwa kile ambacho amekifanya, tunaangalia mkataba wake na vilevile tunakwenda kutoa hukumu ambayo inaendana na sheria za mpira wa miguu” amesema Ahmed
0 Maoni