Hadija Chikundi (30) mkazi wa Tandika wilayani Temeke amehukumiwa miaka 30 kwenda jela baada ya kukutwa na hatia ya kusafirisha madawa ya kulevya aina ya bangi yenye uzito wa Kilo 13.7.
Hukumu hiyo imetolewa na hakimu mkazi mwandamizi wa mahakama ya wilaya ya Lindi Muyonga Magara baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na mashahidi watano ikiwampo ripoti ya mkemia mkuu wa serikali kanda ya Mtwara.
Akisoma hukumu hiyo hakimu Magara alisema "Ripoti ya mkemia mkuu kutoka mtwara imeeleza bayana madhara ya madawa ya kulevya aina ya bangi inaharibu nguvu kazi ya taifa"
Hakimu Magara akitoa hukumu ya kesi hiyo namba 07/2022, kupitia kifungu cha 15 'A' (1) na (2) C Sheria, Sura ya 95, marejeo la mwaka 2019, alisema: "Sheria imenifunga mikono, hivyo ninakuhukumu kwenda jela miaka 30".
Awali ilidaiwa mahakamani huko na Mwanasheria wa Serikali, Mramba kuwa mshtakiwa huyo alikamatwa Februari 27, mwaka huu katika kizuizi cha polisi kilichoko eneo la SIDO, Manispaa ya Lindi, akiwa anasafirisha dawa hizo akitokea Nyangao, Halmashauri ya Mtama kwenda mkoani Dar es Salaam.
Kabla ya kutolewa hukumu hiyo, mshtakiwa alipewa nafasi ya kujitetea, akiiomba mahakama kutompa adhabu bali imwonee huruma na kumsamehe kwa sababu kosa hilo ametenda kwa mara ya kwanza, pia ni yatima.
Pia alijitetea kwamba ana mtoto mdogo anayemlea peke yake kulikosababishwa na mwenza wake kufariki dunia miaka miwili iliyopita.
Baada ya utetezi huo, Hakimu Magara alimuuliza Mwanasheria wa Serikali, Godfrey Mramba kama anazo kumbukumbu za makosa ya zamani dhidi ya mshtakiwa huyo, akijibu hana na kudai kuwa upande wa Jamhuri hauna pingamizi na kuiomba mahakama hiyo kumpa mshtakiwa adhabu kwa mujibu wa sheria inavyoruhusu.
CHANZO; Nipashe
0 Maoni