JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Saalam, limeua vijana sita wanaosadikiwa kuwa ni 'panya road' waliokuwa wanakwenda eneo la Kinzudi, kufanya uhalifu wa kuvamia mtaa na kupora.
Vijana hao ni kati ya tisa waliokamatwa katika mapambano na polisi, kati yao sita walijeruhiwa na kufariki dunia wakati wakipelekwa hospitalini kwa matibabu.
Akifafanua kuhusu tukio hilo jana, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, alisema saa 4:15 usiku juzi, walipata taarifa kutoka kwa wananchi kwamba kuna kikundi cha wahalifu waliokuwa kwenye Noah yenye namba za usajili T 260 BEP wanaotoka Mabibo wakiwa na silaha wakielekea Goba Kinzudi kwa lengo la kufanya uvamizi.
Alisema baada ya kupokea taarifa hizo, ufuatiliaji wa haraka ulianza na askari polisi walipofika eneo la Makongo walikutana na gari hilo na walipolizuia ili kuwakamata wahalifu hao walishuka na kuanza kuwatishia polisi kwa mapanga ili wasikamatwe.
"Katika mazingira hayo askari walijihami kwa kufyatua risasi kadhaa hewani, lakini wahalifu hao waliendelea kukaidi na kutaka kuwajeruhi polisi, ndipo walishambuliwa na kujeruhiwa na baadaye walipelekwa haraka hospitalini, lakini kwa bahati mbaya walipoteza maisha," alisema na kuongeza:
"Wahalifu watatu katika purukushani hizo walifanikiwa kukimbia na Jeshi la Polisi linawasaka na litawakamata haraka iwezekanavyo, uchunguzi wa awali umebaini kuwa watu wawili kati ya wahalifu hao Salum Mkwama (30), mkazi wa Mbagala na Khalfan mkazi wa Buguruni, waliwahi kushtakiwa kwa kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha mwaka 2021 na baadaye kuachiwa kwa sababu mbalimbali za kisheria," alisema Muliro.
Kadhalika, Kamanda Murilo alisema watuhumiwa hao walikutwa na mapanga sita, visu viwili na vifaa vingine vya kuvunjia nyumba, akibainisha kwamba upelelezi wa awali pia umebaini kuwa watuhumiwa hao wanadaiwa kushiriki tukio la mauaji lililotokea Kawe Septemba 14, mwaka huu.
Alisisitiza kuwa jeshi hilo litaendelea kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Camillius Wambura ya kwamba mifumo ya usalama na kisheria inazingatiwa ili kuhakikisha hali ya usalama inarejeshwa haraka iwezekanavyo jijini Dar es Salaam.
0 Maoni