TANGAZA HAPA

Mume amuua mke na kutupa mwili wake

Kamanda wa Polisi Mkoani Dodoma Martin Otieno

Mkazi wa Kata ya Bahi Sokoni, Juma Linoga anadaiwa kumuua mkewe, Mariam Alex (34) kisha mwili wake kuufunika na mifuko ya saruji ndani ya pagale.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martin Otieno alisema jana kuwa mauaji hayo yalitokea Oktoba 15 mwaka huu na mtuhumiwa wa tukio hilo amekimbia.

Alisema mwili wa Mariam uligundulika katika pagale hilo saa 9.30 alasiri baada ya taarifa kutolewa.

“Tuliukuta mwili ukiwa umepigwa na kitu sehemu mbalimbali lakini bado tunafanya uchunguzi kujua chanzo cha mauaji hayo ni nini ili hatua kali zichukuliwe kwa waliohusika,” alisema Otieno.

Kamanda Otieno alisema baada ya mauaji hayo, mtuhumiwa alikimbia na jeshi hilo linaendelea kumtafuta ili ahojiwe.

  • Jela mwaka mmoja kwa kumchoma mikono mwanae kwa kudokoa dagaa

Akisimulia kuhusu tukio hilo, Pili Mbasha alisema baada ya kupata taarifa kutoka kwa mtoto wa marehemu alikwenda nyumbani kwao na hakuwakuta wanandoa hao, lakini akashuhudia miburuzo ndipo akamtaarifu mwenyekiti wa kitongoji.

Alisema kiongozi huyo alipofika, waliongozana naye hadi katika eneo la tukio na kuanza kutafuta huku wakiongozwa na miburuzo ya mwili, lakini hawakufanikiwa kuona kitu wakati mhusika alipobadili mwelekeo na kuubeba mwili kisha akarudi nyuma hadi kwenye pagale alikokwenda kuuficha.

“Tulitumbukia hadi mtoni na kurudi ndani kuangalia lakini hatukufahamu chochote, ndipo tuliwaita polisi kuja kutusaidia na kwa kuwa wenzetu wana mbinu za utafutaji na hisia zao, ndipo mmoja wa askari alipoangalia ndani ya pagale akasema mbona pale kama kuna miguu ya mtu,” alisema Pili.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nkungugu, Pascal Mchela alisema mtoto (wa Mariam), alimweleza kuwa Oktoba 13 Juma alifika nyumbani kwa mkewe usiku na kumuita bila mafanikio, ndipo alipoambiwa na mtoto kuwa inawezekana hajarudi.

Alisema baba yake alimtaka mtoto huyo kwenda nyumbani kwake mapema asubuhi, jambo alilolifanya lakini alipofika aliona damu katika miti karibu na nyumba hiyo na wakati huo hakuwakuta wazazi wake wote.

Mbali na kuona damu, inaelezwa kuwa alihisi kama kuna kitu kilichowekwa mahali lakini wakati wote huo hakuwa ametilia shaka, ndipo akaendelea na shughuli zake, ikiwamo kupeleka maji.


CHANZO:Mwananchi


Chapisha Maoni

0 Maoni