TANGAZA HAPA

Amnyonga mkewe hadi kufa kisha kumfungia ndani

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi.

KASANA Masanja (25) mkazi wa Kijiji cha Kizungu Kata ya Lyamidati wilayani Shinyanga, amedaiwa kuuawa na mume wake, Hamis Katunduru (35), kwa kumnyonga shigo hadi kufariki dunia kisha kumfungia ndani na kuondoka.

Tukio hilo lilitokea juzi majira ya 4:00 asubuhi katika kijiji hicho na mtuhumiwa baada ya kutekeleza mauaji hayo alikimbilia kusikojulikana.

Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Janeth Magomi, akizungumza na Nipashe jana, alisema chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa kimapenzi na kwamba mtuhumiwa tayari ametiwa mbaroni na wanaendelea na upelelezi ili hatua za kisheria zichukuliwe.

"Baada ya bwana huyu kutekeleza mauaji dhidi ya mke wake, alimfungia ndani kisha akaondoka. Lakini majirani zake walianza kuuliza mbona mwanamke mwenzao hawamwoni, ndipo wakaanza kufuatilia na kubainika ameuawa na mume wake na kufungiwa ndani," alisema Magomi.

Alisema polisi baada ya kupata taarifa, walifika eneo la tukio na kuvunja mlango na kumkuta mwanamke huyo akiwa ameuawa. Alisema taarifa za uchunguzi wa daktari wa serikali ilionyesha alinyongwa shingo hadi kufa.

Pia alisema mwili wa marehemu tayari umeshakabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya mazishi.

Diwani wa Lyamidati, Veronica Mabeja, alisema mwanamke huyo aliuawa na mume wake mwezi uliopita akafungiwa ndani, sababu waliukuta mwili wake ukiwa umeanza kuoza.

Alisema walikuta mwili huo ukiwa umeviringishwa kwenye gunia na kufungwa kamba nyingi na alipomhoji mtuhumiwa kwa nini ametekeleza mauaji hayo, alisema mwanamke huyo hajamzalia mtoto.

Diwani huyo alisema kwa taarifa alizozipata kwa majirani zake ni kwamba mwanamke huyo alikuwa akiishi kwa mateso hata mume wake akisafiri alikuwa anamfungia ndani na kujisaidia humo humo hadi arudi kutoka safarini na alipigwa marufuku kwenda kwa majirani.

Alisema siku ya tukio, majirani zake walisikia akipiga kelele kuomba msaada kuwa anakufa na kulipokucha hawakumwona tena hadi juzi ilipogundulika kuwa siku hiyo aliuawa na kufungiwa ndani.

Chapisha Maoni

0 Maoni