Mahakama ya Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa imemhukumu kifungo cha Miaka 30 jela mkazi wa Kijiji cha Ilamba, Neusi Mtasingwa (45) baada ya kukutwa na hatia kwa kosa la kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 14.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Novemba 2, 2022 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo Benedict Nkomola amesema mshtakiwa huyo amehukumiwa adhabu hiyo kwa kosa la ubakaji kwa mujibu wa kifungu 130(1),(2),(e) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura 16 rejeo la mwaka 2022.
Aidha Hakimu huyo ameeleza kuwa siku ya Oktoba 24 mwaka huu majira ya mchana wakati mwathirika wa tukio hilo akiwa katika harakati zake za kuuza maandazi alikutana na mshtakiwa huyo na kununua maandazi hayo na kuchukua mengine matatu na kumuagiza kupeleka nyumbani kwake wote wakiwa wawili wakati wakiwa njiani kuelekea kwa mshtakiwa ndipo alitumia nafasi ya kumshika kwa nguvu na kumvutia kwenye msitu na kumvua nguo zake na kisha kumbaka," ameeleza hakimu huyo.
Nkomola amefafanua kuwa baada ya mtoto huyo kufanyiwa kitendo hicho, hakufurahishwa ndipo alimwambia mama yake Subira Mdemu.
"Baada ya kupata taarifa mama huyo alilifikisha katika vyombo vya sheria na mshtakiwa kukamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Mafinga baada ya kusikilizwa kwa mlalamikaji na kujiridhisha kwamba kuna tukio la ubakaji," amesema hakimu.
Vilevile hakimu huyo amesema kuwa baada mshtakiwa huyo kufikishwa mbele ya Mahakama hiyo Novemba Mosi mwaka huu kwa ajili ya kujibu shtaka lake alikili kumuingilia mtoto huyo.
"Kitendo cha kukili na hati ya maelezo kutoka kwa upande wa mashtaka hivyo mahakama ikamtia hatiani kwa kosa hilo kwa adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela," amesema hakimu huyo.
Mahakama hiyo imetoa hukumu hiyo ya kifungo cha miaka 30 Jela ili iwe fundisho kwa mshtakiwa pamoja na jamii wenye tabia kama hiyo.
0 Maoni