TANGAZA HAPA

Mbaroni kwa madai ya kutekwa na kuporwa milioni 60

Kamishna msaidizi (ACP) Jumanne Muliro

Mhasibu wa Kampuni ya Your Home Choice ya Keko, Dar es Salaam, Deodatus Luhela (35), anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kuwa ametekwa na kujeruhiwa na majambazi kisha kuporwa Sh. milioni 60 za mwajiri wake.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi (ACP) Jumanne Muliro, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa mtuhumiwa alitoa taarifa kituo kidogo cha polisi cha Gongo la Mboto na baadaye kufungua jalada katika Kituo cha Polisi Chang'ombe akidai kufanyiwa kitendo hicho.

Muliro alisema Novemba 14, mwaka huu, mtuhumiwa huyo katika taarifa alizotoa polisi, alidai kuwa majambazi walimjeruhi na kumpora Sh. milioni 60 alizokuwa ametumwa na mwajiri wake kuzichukua katika benki ya CRDB tawi la TAZARA.
Alisema Luhela alidai kuwa siku hiyo, saa 3:30 asubuhi, alikamatwa na majambazi wawili waliokuwa na gari jeusi baada ya kumtishia kwa silaha na baadaye akaingizwa kwenye gari.

Kwa mujibu wa Muliro, mtuhumiwa alidai kuwa majambazi hao walimjeruhi mkono wa kushoto na shavuni na hatimaye kumpora fedha zote alizokuwa nazo.

"Alidai kuwa baada ya tukio hilo alitupwa maeneo ya Gongo la Mboto njia panda ya Pugu na Mbezi, akajikongoja hadi kituo cha Polisi ambako alipewa PF. 3 (Fomu namba tatu ya polisi) kwa ajili ya matibabu. Baadaye mtuhumiwa huyo alifungua kesi ya unyang'anyi na kuporwa Sh. milioni 60 katika kituo cha Polisi Chang'ombe," alisema Muliro.

Baada ya taarifa hizo, Muliro alisema polisi walimhoji kwa kina na kubaini kuwa taarifa hizo zilikuwa za uongo.

Alisema ilipofika Novemba 15, saa 8:00 mchana, mtuhumiwa aliwaongoza askari hadi Chanika Kitunguu, jijini Dar es Salaam, alikokuwa ameficha fedha hizo.

 

Chapisha Maoni

0 Maoni