TANGAZA HAPA

Mwenyekiti akutwa amekufa

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro Kamishna Msaidizi (ACP) Simon Maigwa

Geofrey Massawe mwenyekiti wa kitongoji cha Somanga wilaya ya Hai mkoa wa Kiliamnjaro amekutwa akiwa amefariki huku mwili wake kukutwa ukining'inia juu ya mti.

Inaelezwa kuwa mwili wa Mwenyekiti huyo, ulikutwa juu ya mti wa mparachichi ukiwa na kamba ya kufungia ng'ombe.

Jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi (ACP) Simon Maigwa, alithibitisha kuwa mwili wa Massawe ulikutwa kwenye mti huo Novemba 2, mwaka huu, majira ya asubuhi.

"Ni kweli mwili wake ulikutwa juu ya miti wa mparachichi lakini tunasubiri taarifa ya 'postmortem' (taarifa ya uchunguzi wa kitabibu) ya nini kimemuua.

"Katika uchunguzi wetu wa awali, marehemu hakuacha ujumbe wowote kuhusu alichokifanya. Kwa hiyo hivi sasa makachero wetu wanaendelea na uchunguzi dhidi ya kifo hicho," alisema.

Mmoja wa wakazi wa Somanga, Sospeter Uronu, alisema alimwona Massawe kabla ya kifo chake akiwa na kamba na alipomwuliza anakwenda wapi, alimjibu anakwenda kukata majani ya mbuzi.

"Hapa kwangu si mbali na nyumbani kwake. Jana (juzi) asubuhi nilimwona akiwa na kamba akaniambia anatafuta majani ya mifugo yake, lakini muda mfupi baadaye tulipata taarifa kwamba kuna mtu amejinyonga na tulipofika tulikuta ni ndugu yetu, inauma sana,"alisema.

Alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Sawe, Penda Kimaro, alisema alipigiwa simu na wananchi na kutaarifiwa kwamba wamemkuta mtu akiwa ananing'inia juu ya miti, huku kamba ikiwa shingoni.

"Baada ya kupata tu hiyo taarifa, niliita Polisi wa Kituo cha Polisi Bomang'ombe na walipokuja walimchukua na kumpeleka Zahanati ya Masama kwa ajili ya kumhifadhi,"alieleza. 

CHANZO: Nipashe

Chapisha Maoni

0 Maoni