TANGAZA HAPA

Wafukua kaburi na kunyofoa viungo


Watu wasiojulikana wamefukua kaburi la Neema Mlomba (26) wa Kijiji cha Luteba, Halmashauri ya Busokelo wilayani Rungwe ambaye alifariki dunia kwa matatizo ya uzazi na kisha kunyofoa baadhi ya viungo vya mwili wake na kuondoka navyo.

Baadhi ya viungo vilivyonyofolewa kwenye mwili wa mwanamke huyo ni ulimi, moyo, kiganja cha mkono wa kulia, titi la kulia, mdomo na jicho la kulia.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, alisema kabla ya kufikwa na umauti, mwanamke huyo alifika katika Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Mbeya kitengo cha Wazazi Meta, kwa ajili ya kujifungua.

Homera alisema kwa bahati mbaya mwanamke huyo alifariki dunia Novemba 5, mwaka huu, wakati akijifungua ingawa mtoto aliyezaliwa alipona na yuko katika hospitali hiyo chini ya uangalizi wa madaktari.

Alisema mwili wa mwanamke huyo ulichukuliwa na ndugu zake na kwenda kuzikwa kijijini kwao Luteba Novemba 6, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Homera, asubuhi ya Novemba 7, mwaka huu, kaburi lililozikwa mwili wa marehemu lilikutwa limefukuliwa na mwili ukiwa nje ya kaburi umenyofolewa baadhi ya viungo.

"Tukio hili la kufukuliwa kwa mwili wa marehemu na watu wasiojulikana linaonekana lilifanyika usiku wa manane wa kuamkia Novemba 7, mwaka huu. Asubuhi wananchi walikuta kaburi hilo likiwa limefukuliwa na baadhi ya viungo kunyofolewa," alisema Homera.

Alisema tukio hilo linahusishwa na imani za kishirikina, ingawa mpaka sasa watu waliohusika na ukatili huo bado hawajafahamika.

Mkuu huyo wa mkoa aliliagiza Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa haraka ili kuwabaini watu walifanya tukio hilo ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Alisema katika siku za hivi karibuni, Wilaya ya Rungwe imekuwa na matukio mengi ya kusikitisha yakiwamo mauaji na watu kujichukulia sheria mkononi.

Homera aliwataka wananchi wa mkoa wa Mbeya kuachana na imani za kishirikina kwa kuwa hayana tija kwa maendeleo na maisha yao na mkoa wa kwa ujumla.

"Matukio ya aina hii yanautia aibu mkoa wetu wa Mbeya. Nitoe rai kwa wananchi kuachana na imani za kishirikina na pia watoe ushirikiano kwa vyombo vyetu vya dola ili kukomesha tabia hizi," alisema.

Akizungumzia hali ya mtoto aliyezaliwa kabla ya mama yake kupoteza maisha, Homera alisema mtoto huyo yuko chini ya uangalizi wa madaktari na hali yake inaendelea vizuri.

Chapisha Maoni

0 Maoni