TANGAZA HAPA

Zumaridi adai kuibiwa milioni 19 siku aliyokamatwa na polisi

Mshtakiwa Diana Bundala maarufu kama zumaridi

Mshtakiwa  Diana Bundala (40), maarufu Mfalme Zumaridi, amedai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza kuwa wakati wa ukamataji wa askari katika chumba chake, zimeibwa Sh. milioni 19.5 na simu mbili baada ya yeye kutolewa nje.

Alidai hayo mahakamani huko jana alipowasilisha utetezi wake katika kesi inayomkabili na wenzake 83, kuhusu utata wa saini yake katika maelezo ya onyo.

Zumaridi alidai kuwa siku ya tukio hilo, alivamiwa na askari waliokuwa hawajavalia sare za polisi kinyume cha maelezo yaliyowasilishwa mahakamani.

Mshatikiwa huyo namba moja alidai kuwa kipindi cha ukamataji Februari 26 mwaka huu, askari walimvamia katika chumba chake na kumtoa nje huku wao wakiendelea kukagua chumbani huko bila kuwapo kwake.

Alidai askari hao hawakusema sababu ya ukaguzi huo pamoja na kutolewa nje, hatua iliyosababisha askari hao kuchangia upotevu wa fedha hizo na mali zake nyingine ndani ya chumba chake.

Shahidi mwingine katika kesi hiyo, Neema Julian (36) alidai askari walipofika eneo hilo, walivamia nyumba hiyo na kupiga mabomu ya machozi pamoja na kupiga watu waliokuwamo kwenye ngome hiyo, kitendo kilichozua taharuki kwa waumini hao.

Shahidi mwingine, Diana Michael (26) alidai wakati anafika katika eneo hilo, alikuta askari hao wameishavamia eneo hivyo naye alianza kushambuliwa na askari hao baada ya kujulikana kuwa ni miongoni mwa waumini.

Kesi hiyo iko chini ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Clescensia Mushi ambaye anatarajiwa Novemba 9 mwaka huu kutoa uamuzi kuhusu utata ulioibuka ili kuendelea na ushahidi wa kesi ya msingi.

CHANZO: NIPASHE


Chapisha Maoni

0 Maoni