TANGAZA HAPA

Mbaroni kwa kumuozesha mwanafunzi


Jeshi la Polisi mkoani Mtwara linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kumwozesha mwanafunzi wa kidato cha kwanza mwenye umri wa miaka 16 (jina linahifadhiwa).

Watu hao, wakazi wa Kijiji cha Shaba, Kata ya Mtimbwilimbwi, Halmashauri ya Nanyamba, wanadaiwa walipanga ndoa hiyo kufungwa usiku ili waoaji na familia ya mwanafunzi wafanikishe mpango huo bila kufahamika, huku ikidaiwa kuwa ilihudhuriwa na watu wachache.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Kamishna Msaidizi Nicodemus Katembo, aliwaambia waandishi wa habari  kuwa tukio hilo lilitokea Desemba 12 mwaka huu, kwenye kijiji hicho majira ya saa nne usiku.

Alisema kuwa usiku wa siku hiyo, Radhamani Saidi (38) ambaye ni baba wa mwanafunzi huyo, akishirikiana na mzazi mwenzake, Mwajuma Chilungu (34), mkazi wa Magomeni mkoani Mtwara, walimwozesha mtoto wao ambaye ni mwanafunzi wa sekondari huku wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Kamanda Katembo alisema wazazi hao walimwozesha mwanafunzi kwa Hamisi Chiwandi, mkazi wa Charambe mkoani Dar es Salaam na kwamba katika ndoa hiyo, bwana harusi aliwakilishwa na Radhamani Lingwala, mkazi wa Magomeni, Mtwara.

Alisema kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi linawashikilia watu hao watatu ambao ni baba, mama wa mwanafunzi huyo pamoja na mwakilishi wa bwana harusi.

Alisema polisi wanaendelea na utaratibu wa kisheria na kwamba watu hao watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kumwozesha mwanafunzi.

Baadhi ya ndugu na majirani wa mwanafunzi huyo, waliiambia Nipashe kuwa walishangazwa kuona mwanafunzi huyo akifunga ndoa huku akiwa anasoma na kujiuliza imekuwaje wazazi wake wameridhia ndoa hiyo kufungwa.

Saidi Machapa, babu wa mwanafunzi huyo, alidai kuwa alipoona mchakato wa mjukuu wake kutaka kuolewa, alimwita na kukaa naye na kumuuliza sababu za kutaka kuolewa wakati bado mwanafunzi na akajibiwa kuwa ameshaacha shule ndiyo maana anataka kuolewa na haoni sababu ya kutokuolewa.

Alisema alimsihi mjukuu wake kuachana na mpango huo wa kutaka kuolewa na kuendelea na masomo lakini mwanafunzi huyo alikataa na kumweleza kinagaubaga kwamba hayuko tayari kuendelea na masomo.

Shangazi wa mwanafunzi huyo, Rukia Machapa alisema mwanafunzi alikataa ushauri wa ndugu zake ambao walimshauri kutokukubali kuolewa akiwa bado mwanafunzi na sheria hairuhusu mwanafunzi kuolewa.

"Tulipomshauri alisema hataki shule, anataka kuolewa na kama wazazi wataendelea kumkataza kuolewa, basi atalazimisha kushika ujauzito na mpenzi wake anayetaka kumuoa ili aone kama wazazi wataendelea kumkataza kuolewa na pia atatoroka kwenda Dar es Salaam kwa mpenzi wake," alidai Rukia

 

Chapisha Maoni

0 Maoni