TANGAZA HAPA

Ajeruhiwa kwa kumwagiwa Tindikali na watu wasiojulikana

mtzonline255

Jeshi la Polisi Mkoani Katavi limesema kuwa mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Ernest Lyoba (61) Mkazi wa Kijiji cha Namanyere Kata ya Majimoto Wilaya ya Mlele amejeruhiwa vibaya katika sehemu yake ya uso na mgongoni baada ya kumwagiwa tindikali na watu wasiojulikana.

Hayo yamebainishwa na Kamanda wa Polisi mkoani Katavi, Kaster Ngonyani wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema tukio hilo limetokea June 25,2023 huko katika eneo la Kijiji cha Namanyere wakati mtu huyo akiwa njiani akielekea nyumbani kwake .

Kamanda Ngonyani amebainisha kuwa siku ya tukio Ernest alikuwa yuko njiani akiwa anaelekea nyumbani kwake majira ya saa tisa alasiri mara baada ya kuwa amemaliza shughuli zake za kujitafutia riziki ndipo watu wasiojulikana walimmwagia tindikali sehemu za usoni na mgongoni na kumjeruhi vibaya na kisha watu hao walitokomea mahali pasipojulikana.

Kamanda Ngonyani amesema baada ya mwathirika wa tukio hilo kumwagiwa tindikali hiyo alipiga kelele za kuomba msaada na muda mfupi watu walifika kwenye eneo hilo na kumkuta Ernest akiwa amejeruhiwa vibaya .

Ameeleza kuwa wasamaria wema hao walimchukua na kumkimbiza haraka hospitali ya Halmashauri ya Mpimbwe kwa ajiri ya matibabu hata hivyo kutokana na kuwa amejeruhiwa vibaya mgonjwa alipewa rufaa ya kwenda kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi.

Amesema baada ya kuwa amefikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi alipewa tena rufaa ya kwenda kupatiwa matibabu zaidi kwenye Hospitali ya Rufaa ya KCMC ya Mkoani Kilimanjaro ambako amelazwa hadi sasa.

Amesema juhudi za kuwanasa watuhumiwa hao zinaendelea kufanywa na jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi ili kuhakikisha linawakamata na kuwatia nguvuni na kuwafikisha mara moja Mahakamani ili kujibu mashitaka ya tuhuma zitakazokuwa zinawakabili.

Chapisha Maoni

0 Maoni