Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mara imemuhukumu kwenda jela miaka saba Msirari Muhere (60) mkazi wa Wilaya ya Tarime baada ya kupatikana na hatia ya kumuambukiza ugonjwa wa Ukimwi mtoto wa miaka sita kwa makusudi.
Hukumu hiyo imetolewa jana Mei 31, 2023 na Hakimu Mkazi Mkuu mwenye mamlaka ya ziada ya kusikiliza mashauri ya Mahakama Kuu, Timoth Swai, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo.
"Ushahidi umeonyesha kuwa Muhere alichukua sindano na kunyonya damu kutoka kwa mtoto wa mke wake mkubwa ambaye alikuwa ameathirika kisha kuanza kuwadunga watoto wawili wa huyu mke wake wa pili na uchunguzi wa kitabibu umebaini kuwa kati ya hao watoto wawili mmoja wa kiume ameambukizwa ugonjwa wa Ukimwi," amesema.
"Muhere na mke wake mkubwa ni waathirika wa Ukimwi na binti yao alizaliwa na ugonjwa huo kwa hiyo baada ya kutofautiana na mke mdogo aliamua kumkomesha kwa kuwaambukiza watoto wake Ukimwi labda kwasababu hawakuwa wa kwake (Muhere) wa kuzaa," ameongeza.
0 Maoni