Watu watatu wamejeruhiwa kwa kukatwa katwa mapanga sehemu mbambali ya miili yao baada ya watu wasiojulikana kuvamia nyumba moja yenye duka, baa na vyumba vya kulala wageni katika Kijiji cha Bisumwa Wilaya ya Butiama mkoani Mara.
Majeruhi hao ,Majuto Masanje, Amos Kiturugu na Hussein Muremwa wamelezwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara mjini Musoma huku Majuto akiwekwa kwenye uangalizi maalum (ICU)
Mmoja wa majeruhi hao ambaye ni mmiliki wa nyumba hiyo, Amos Kiturugu amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Juni Mosi, 2023 katika kijiji cha Bisumwa.
Amesema akiwa amelala ndani alisikia kama kuna watu wanapigana nje lakini alipochungulia dirishani alisikia sauti za watu hao wakisema kuwa ni askari polisi wapo doria.
"Niliposikia kuwa ni maaskari nikafungua mlango na geti nikatoka nje ile natoka tu wakawasha tochi tatu na kunitaka nikae chini ya ulinzi,"
"Nilikaa chini ya ulinzi nikawa nawaangalia ili niweze kuwoana vizuri lakini nilichoona walikuwa wamebeba mapanga na nondo nikasema hawa sio askari polisi,"amesema
Amesema baada ya kutii amri hiyo watu wanne akiwepo mwanamke mmoja walimsogelea na kumtaka awapeleke walipo wahudumu wa baa agizo ambalo aliltii huku wengine wakibaki nje.
Amesema baada ya kuwapeleka walipo wahudumu watu hao walianza kuamuru wapewa hela kisha kumshambulia kwa kumpiga na nondo kisogoni na ubavuni kabla ya kuhamia kwenye duka lake na kuanza kutafuta hela.
"Waliingia dukani na kuvuruga wakiwa wanatafuta hela na wameondoka na Sh700,000 zilikuwepo za mauzo na marejesho ya pikipiki pia wameondoka baadhi ya vitu vya dukani" amesema
Majeruhi mwingine, Hussein Muremwa amesema kuwa akiwa amelala kwenye chumba cha wageni aliskia kelele nje na baada ya kubaini kuwa wamevamiwa ailiingia uvunguni kwaajili ya kujinusuru.
"Walifungua mlango wakamulika uvunguni wakaniambia jiyine nilivyotika wakanipiga na kitu shingoni mwa nyuma wakaniambia niwape hela nikawapa Sh12,000 nilizokuwa nazo wakanipiga tena kisha wakatoka nje" amesema
Daktari wa Idara ya Upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, Dk Charles Paschal amesema majeruhi wawili wanaendelea vizuri na kwamba wanaweza kuruhusiwa kutoka hospitalini kesho.
"Huyu mwingine hali yake sio nzuri amekatwakatwa na kitu chenye ncha kali kichwani na kupelekea kupoteza damu nyingi kwahiyo tumemfanyia upasuaji lakini bado anatakiwa aende kwenye CT- Scan ili kujua kama ubongo umeathirika," amesema Dk Paschal
Amesema hivi sasa wanaangalia maendeleo ya mgonjwa huyo na kwamba upo uwezekano wa kupewa rufaa kesho kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando kwa uchunguzi zaidi.
Katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita Mkoa wa Mara hasa wilaya za Butiama na Tarime zimekumbwa na matukio ya mauaji na uhalifu wa kutumia silaha.
Tukio la hivi karibuni lilitokea Mei 28, 2023 usiku katika vijiji vya Nyakiswa na Nyamikoma wilayani Butiama ambapo madereva boda boda wanne waliuwawa kwa kupigwa na vitu vyenye ncha kali sehemu mbalimbali ya miili yao hasa vichwani
Kamanda wa polisi mkoa wa Mara, Salum Morcase hakupatikana kuzungumzia tukio hilo kwa maelezo kuwa yupo njiani.
"Niko barabarani naenda Lamadi mpaka nikitulia kwasasa siwezi kuongea,"amesema kupitia simu ya mkononi
0 Maoni