Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linamshikilia Meshack Azikam (23) kwa tuhuma za wizi wa misalaba 14 ya chuma inayosemekana ameiong’oa kwenye makaburi ya Kola Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa mwishoni mwa wiki akiwa anang'oa msalaba katika makaburi hayo na polisi walipokwenda kumpekua nyumbani kwake walikuta misalaba 13 ambayo alikuwa amepanga kuifuta majina na kuuza kama chuma chakavu.
Kamanda Mkama amesema kuwa jitihada za kumkamata mtuhumiwa huyo zilitokana na taarifa zilizotolewa na baadhi ya ndugu waliokuwa wamewazika wapendwa wao katika makaburi hayo hivyo polisi iliweka mtego na kufanikiwa kumnasa mtuhumiwa huyo ambaye ni mkazi wa Kichangani Manispaa ya Morogoro.
"Watu wanapokwenda kuzulu makaburi ya wapendwa wao wamekuwa wakikuta makaburi hayo yakiwa hayana misalaba, malalamiko hayo yalitufukia na sisi kama Jeshi la Polisi tulianza kufanya misako yetu ambayo imefanikisha kukamatwa Kwa mtuhumiwa huyo," amesema Kamanda Mkama
Kufuatia tukio hilo baadhi ya viongozi wa dini ya Kikristo wamelaani na kuliomba Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote wanaojihusisha na wizi wa misalaba.
Mmoja wa viongozi hao ni pamoja na mratibu wa Kanisa Kuu Katoliki Jimbo la Morogoro, Cosmas Kigona ameeleza kuwa Kanisa hilo linalaani kitendo cha wizi wa misalaba kwani amesema kuwa mbali ya kutumika kama alama pia inatumika kwa kiimani
"Msalaba ni imani kwetu, hawa wanaoiba misalaba ni ishara wazi kuwa watu hawa hawana hawana hofu ya Mungu, hawajui kama nao ipo siku watakufa na watawekewa misalaba," amesema Kigona.
Naye Mzee wa Kanisa la KKKT, Pascal Mataba ameliomba Jeshi la Polisi kuhakikisha mtuhumiwa huyo anafikishwa mahakamani ili iwe fundisho kwa wengine wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Hata hivyo amesema kuwa kwa sasa ipo haja ya kutafuta namna nyingine ya kuweka alama kwenye makaburi ikiwa ni pamoja na kuweka misalaba inayotengenezwa kwa kutumia zege.
0 Maoni