Mahakama Kuu Kanda ya Tabora imewahukumu kunyongwa hadi kufa washtakiwa wanne wakazi wa Kata ya Usunga Wilaya ya Sikonge kwa kosa la kumuuwa Alfred Lusamalo aliyekuwa Diwani (CCM) miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa 2020.
Waliohukumiwa kunyongwa ni Nelson Mlela (37), Masemba Lusangija (36), Ramadhani Saidi (29) na Abdallah Habibu (30).
Akitoa hukumu hiyo Juni 19, 2023, Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Tabora, Jovit Kato aliyekasimiwa kusikiliza mashauri ya mauaji amesema washtakiwa hao walitenda kosa la mauaji Machi 6, 2020.
Amesema waliosababisha kumuua Diwani huyo ni Masemba Lusangija ambaye alikuwa msimamizi wa mifugo yake na Nelson Mlela akiwa mwenyekiti wa Serikali ya kijiji ambaye alikuwa anataka kugombea udiwani katika kata hiyo.
Hakimu Kato amesema washitakiwa hao walikuwa wakienda nyumbani kwa marehemu mara kwa mara wakiwa wanajipanga kwenda kufanya mauaji ya diwani huyo.
Amesema mshitakiwa Masemba Lusangija alikuwa na tamaa ya kumiliki mifugo ya marehemu ambayo aliyokuwa akiichunga huku Nelson Mlela akiwa na tamaa ya kupata madaraka ya udiwani nafasi iliyokuwa inashikiliwa na marehem Alfred.
Amesema washtakiwa wote walikwenda kukaa darajani wakimvizia marehemu kwa kuwa alikuwa mnywaji wa pombe na kufanikiwa kumpata wakati anarudi nyumbani kwake kisha kumuua kwa kumkata mapanga.
Awali Mawakili Upande wa Jamhuri wakiongozwa na Alis Thomas na Steve Mzava, waliiambia Mahakama hiyo itoe adhabu kali kulingana na tukio hilo la mauaji.
Upande wa utetezi ukiongozwa na Amos Gehese akisaidiana na Agnes Simba waliiomba Mahakama itende haki kutokana na kosa lao ili iweze kuwa fundisho kwa watu wengine wenye nia kama hiyo.
0 Maoni