TANGAZA HAPA

Watu 41 wauawa katika ghasia kwenye jela ya wanawake

Takriban watu 41 wameuawa katika ghasia katika gereza la wanawake nchini Honduras siku ya Jumanne.

Inafahamika kuwa mapigano yalizuka kati ya magenge hasimu, ambapo genge moja liliwasha moto katika seli.

Maafisa wanasema moto huo ulisababisha vifo vingi lakini baadhi ya waathiriwa walipigwa risasi

Naibu Waziri wa Usalama wa nchi hiyo, Julissa Villanueva, ametangaza hali ya hatari na kuahidi kukabiliana na ghasia hizo.

Pia aliidhinisha "kuingilia kati mara moja" kwa wazima moto, polisi na wanajeshi.

"Hasara ya maisha ya binadamu haitavumiliwa," Bi Villanueva alisema.

Haijulikani ikiwa wote waliouawa walikuwa wafungwa wa jela hiyo, ambayo iko takriban kilomita 20 kutoka mji mkuu wa Honduras, Tegucigalpa, na inashikilia karibu watu 900.

Wafungwa wengine kadhaa wamepelekwa hospitalini.

Delma Ordonez, ambaye anawakilisha wanafamilia wa wafungwa, aliviambia vyombo vya habari vya ndani sehemu ya gereza "imeharibiwa kabisa" katika ghasia hizo.

Video zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha wingu kubwa la moshi wa kijivu ukipanda kutoka kwa gereza la wanawake.

Chapisha Maoni

0 Maoni