Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ametengua uteuzi wa Meneja wa Maji Mkoa wa Dodoma, (Ruwasa) Mhandisi jana Jumanne Juni 21, 2023 kutokana na kile kilichoelezwa kushindwa kutekeleza majukumu yake.
Katika taarifa iliyotumwa kwa umma na wizara hiyo inaeleza kuwa mbali na utenguzi huo, Aweso ametoa maelekezo ya kuundwa timu ya wataalam kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maji mkoani hapo.
“Waziri Aweso amemuelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba kuunda timu ya wataalam ya kufuatilia changamoto ya utekelezaji wa miradi ya maji mkoani Dodoma na kutoa suluhisho la kumaliza changamoto hizo mara moja,”imeeleza taarifa hiyo.
Vilevile, ameelekeza timu hiyo ya wataalam itakayoundwa na Katibu Mkuu ifanye tathimini ya utendaji kazi wa mameneja wa wilaya zote wa maji vijijini (Ruwasa) Mkoa wa Dodoma.
Ziara ya Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo huenda ikawa sababu ya kumuondoa Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini (Ruwasa) wa mkoa wa Dodoma Godfrey Mbabaye.
Uamuzi wa Aweso umekuja wakati Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo akiwa amebakiza wilaya mbili kuhitimisha ziara yake mkoani Dodoma huku maeneo mengi kukiwa na lawama za kutoridhishwa na kasi ya upelekaji wa huduma za maji na usimamizi wa miradi hiyo.
Hata hivyo jana Juni 20, 2023 Chongolo alionyesha kuchukizwa na kitendo hicho huku akiahidi kuwa atapeleka taarifa kwa mamlaka za uteuzi na kueleza ukweli halisi wa mambo yalivyo katika miradi ya maji mkoa mzima.
"Hatuwezi kupewa dhamana tukaja kuwapiga hadithi wananchi, hatuwezi kukaa tukabembelezana kwa mambo ya msingi, wananchi mnataka matokeo na sisi tuliahidi kuyatatua sasa kama mtu hataki kuyafanyia kazi aende akalime kwao asikae kwenye nafasi ya kushughulikia matatizo ya wananchi,”alisema Chongolo jana akilalamikia mradi wa maji Kata ya Chandama wilaya ya Chemba.
Akiwa wilaya ya Mpwapwa alikutana na tatizo kama hilo katika Kata za Lupeta, Kingiti na Pwaga na kuagiza akutane na Waziri Aweso katika eneo hilo.
Wilayani Kongwa katika Kata ya Mtanana wananchi walizuia msafara wa Chongolo na kumpokea kwa mabango huku pia kilio kama hicho kilikuwa Kibaigwa.
0 Maoni