Iran imewanyonga wanaume wawili mapema leo kufuatia shambulio dhidi ya Washia na kusababisha vifo vya takribani watu 13 mwezi Oktoba mwaka jana, vyombo vya habari vya serikali ya Iran vimeripoti.
Shirika rasmi la habari la IRNA limesema wawili hao walinyongwa alfajiri katika mji wa kusini wa Shira.
Wakati wa kesi yao wanaume hao walisema kwamba walikuwa wakiwasiliana na Islamic State katika nchi jirani ya Afghanistan na kusaidia kupanga shambulio la madhabahu ya Shah Cheragh huko Shiraz, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Iran.
Picha za CCTV kwenye runinga ya serikali zilionyesha mshambuliaji akiingia kwenye hekalu maarufu baada ya kuficha bunduki kwenye begi na kufyatua risasi huku waumini wakijaribu kukimbia na kujificha.
Mshambuliaji huyo, aliyetambuliwa kuwa raia wa Tajikistan, baadaye alifariki katika hospitali kutokana na majeraha aliyoyapata wakati wa shambulio hilo.
Awali maofisa walisema watu 15 waliuawa katika shambulio hilo, lakini baadaye walirekebisha idadi hiyo hadi 13.
Islamic State, ambayo wakati fulani ilikuwa tishio la usalama katika Mashariki ya Kati, imekiri kuhusika katika ghasia nchini Iran, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya mauaji ya mwaka 2017 ambayo yalilenga bunge na kaburi la mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu, Ayatollah Ruhollah Khomeini.
0 Maoni