TANGAZA HAPA

Mahakama yaamuru kutaifishwa kwa mali za mfungwa

mtzonline255

Mahakama Kuu Divisheni ya Uhujumu Uchumi, imeridhia maombi ya utaifishaji mali za mfungwa Yanga Omari Yanga ikiwemo viwanja vyake saba kufuatia maombi ya Mkurugenzi wa Mashtaka dhidi ya mfungwa huyo kuomba mali zake zitaifishwe.

Uamuzi huo uliotokana na shauli namba 1/2021 uliotolewa hivi karibuni na Jaji Elinaza Luvanda baada ya kuridhika kuwa mali za mshtakiwa huyo ni mazalia ya uhalifu uliotokana na kosa la usafirishaji wa dawa za kulevya.

Mwaka 2020 mfungwa Yanga Omari Yanga alihukumiwa na Mahakama hiyo kutumikia kifungo cha miaka 30 gerezani baada ya kukutwa na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 1052.63.

Akisoma uamuzi huo Jaji Elinaza Luvanda alisema sheria inaelekeza kuwa mali zote zinazopatikana kwa njia ya uhalifu ni lazima zitaifishwe ili kutoa fundisho kwa jamii kuwa uhalifu haulipi.

Mali zilizotaifishwa na Mahakama ni Kiwanja No, 32 Block “C” Magaoni Tanga, Kiwanja namba 73 Block “A” Mwambani Tanga, Kiwanja No. 144 Block “B” Mwakidila Tanga, kiwanja namba 615 na namba 617 Block “B” Kange Tanga, Kiwanja namba 30 Block “C” Mwakidila/Magoani Tanga, kiwanja namba 605 Block “A” Mwambani Tanga na kiwanja namba 606 Block “A” Mwambani Tanga.

Mali hizo zote zipo mkoani Tanga alipokuwa anaishi mfungwa huyo.

Wakati wa usikilizwaji wa shauli hili, upande wa Jamhuri uliwakilishwa na wakili wa serikali Mwandamizi Sabrina Joshi na upande wa utetezi uliwakilishwa na Wakili Nehemia Mkoko

Chapisha Maoni

0 Maoni