Jeshi la Polisi Mkoa wa shinyanga linamtafuta Amos Samson (65) mkazi wa kata ya Kolandoto Manispaa ya Shinyanga kwa tuhuma za kumpa ujauzito mwanafunzi wa kidato cha kwanza mwenye umri wa miaka (16).
Mwanafunzi huyo amedai amepewa ujauzito na mzee huyo baada ya kumshawishi kwa kumpa shilingi 2000 na kumwingilia kimwili kisha kupewa tena shilingi 5000 alipomuita nyumbani kwake na kufanya nae kitendo hicho.
Ameongeza kuwa aliendelea kuwa katika mahusiano ya kimapenzi na mzee huyo tangu Desemba 2022 mpaka alipobainika kuwa na ujauzito unaokadiriwa kuwa na miezi mitano.
Amedai mahusiano yao yalibainika baada ya mzee huyo kumtaka kimapenzi ndugu yake jambo ambalo alichukizwa nalo na kuamua kufichua siri hiyo.
Akizungumza kamanda wa Polisi wa mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi amesema polisi wanaendelea kumtafuta mtuhumiwa huyo anayedaiwa kutoroka huku Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga Dkt Luzila John akithibisha kuwa binti huyo ni mjamzito wa miezi mitano.
Chanzo: Mwananchi
0 Maoni